HAKUNA UCHAWI KATIKA KILIMO – WAZIRI MKUU

Sunday, May 10, 2009

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

HAKUNA UCHAWI KATIKA KILIMO – WAZIRI MKUU
*Ataka Wana Rukwa waache imani za kishirikina mashambani
*Asema siri ni kufuata kanuni bora za kilimo

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema hakuna uchawi wala kulogana katika kilimo na kuwataka wanaRukwaa waachane na imani za kishirikina kwamba mtu anaweza kuvuta mazao kutoka shamba la mwingine na kuyahamishia kwake.

Alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti jana (Jumapili, Mei 10, 2009) wakati akizungumza na wakazi wa kata za Mpui na Miangalua wilayani Sumbawanga, Rukwa ambako anakagua shughuli za maendeleo.

Akiwa Mpui, Waziri Mkuu alisema ni aibu katika karne ya 21 kukuta watu wakiendelea kuamini kuwa mtu akiumwa au akifa basihakuna sababu sababu nyingine isipokuwa kalogwa.

“Achaneni na imani za kuona shamba la mwenzio limestawi hamuoni sababu nyingine eti kavuta mazao yako na kuhamishia shambani kwake... hakuna kitu kama hichokatikakarne hii, cha msingi ni kupanda kwa wakati, kupalilia na kuvuna kwa wakati; na kama ni afya fuateni kanuni za afya hamtapata magonjwa,” alisisitiza.

Akiwa Miangalua ambako alizindua shule ya sekondari ya kata, Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa elimu ili kujikomboa na fikra za uchawi ambazo wengi wamekuwa nazo miaka kwa miaka. “Ni lazima sisi wana-Rukwa tuondokane na hizo imani kwa sababu hakuna kitu kama uchawi, tukazanie masuala ya elimu kwani ndiyo itafumbua fikra...”

Akionyesha kuguswa na matokeo ya shule hiyo, Waziri Mkuu aliamua kumdhamini masomo mwanafunzi pekee aliyemaliza kidato cha nne mwaka jana na kupata daraja la kwanza. Matokeo hayo ni ya kwanza kwa shuke hiyo tangu ianzishwe miaka minne iliyopita.

Kijana huyo, Elias Kalulu alichaguliwa kwenda kidato cha tano katika shule ya sekondari Tosamaganga ambako anasomea masomo ya Fizikia, Jiografia na Hisabati (PGM). “ Huyu kijana amenifurahisha sana... nitamlipia ada hadi amalize kidato cha sita na aende kozi yoyote anayotaka.”

Kabla shule hiyo haijajengwa, watoto wa kata hiyo walikuwa wakienda kusoma katika shule ya sekondari ya kulipia ya Laela iliyoko umbali wa kilometa 15 ambayo inamilikiwa na Kanisa Katoliki.

Mapema, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bw. John Malingula alimweleza Waziri Mkuu kwamba shule hiyo yenye wanafunzi 342, bado inahitaji kukamilisha mabweni kwa vile yaliyopo hayatoshi na pia wanapanga kujenga maabara mbili.

Ili kuunga mkono juhudi wa wananchikatika ujenzi wa shule hiyo, mke wa Waziri Mkuu, mama Tunu Pinda alichangia sh. milioni tano na kuwasisitiza wanafunzi wa kike wa shule hiyo wajitahidi katika masomo na wasikubali kuolewa mapema.

Leo Waziri Mkuu atakwenda Kilyamatundu na Sakalilo wilayani Sumbawanga ambako atakagua mradi wa umwagiliaji na kuzungumza na wananchi wa kata hizo.


(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, MEI 11, 2009.

0 comments:

Post a Comment

About This Blog

Blog Archive

  © Blogger template Noblarum by Ourblogtemplates.com 2009

Back to TOP