WAZIRI MKUU AGAWA MIPIRA, JEZI ZA SOKA WILAYANI MPANDA

Friday, May 15, 2009

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

WAZIRI MKUU AGAWA MIPIRA, JEZI ZA SOKA WILAYANI MPANDA

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ametoa mipira 13 na seti 16 za jezi za mpira wa miguu kwa kata za wilaya ya Mpanda ambazo zimetolewa na kampuni ya simu ya VODACOM.

Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo kutoka kwa Meneja wa Vodacom kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bw. Jackson Kiswaga, Waziri Mkuu alisema ameamua kugawa jezi hizo na mipira katika wilaya nzima ili kuimarisha michezo wilayani humo.

Alisema ameamua kuwaita wadau kutoka majimbo yote matatu ya wilaya hiyo ili wao ndiyo waamue jinsi ya kugawana kwa vipaumbele kwani wilaya nzima ina kata 29 lakini vifaa vilivyopatikana vitatosha kata 16 tu.

“Ninawomba Mwenyekiti na Meya kila mmoja akae na wadau wake na kuangalia njia muafaka ya kugawana hicho kidogo kilichopatikana,” alisema

Alisema ameamua kutoa jezi seti tano na mipira saba kwa ajili ya jimbo la Mpanda Magharibi ambako kuna kata saba; seti nyingine tano za jezi na mipira sita kwa jimbo la Mpanda Kati ambako kuna kata sita na jezi seti sita zilizobaki zitagawiwa jimbo la Mpanda Mashariki ambalo ni la kwake na lina kata 16. Hakuna mipira iliyotolewa kwa jimbo hili.

“Nimeongea na Mkuu wao, na kuwaomba watusaidie kwa ajili ya kata hiyo 13 zilizobaki, wamekubali kwa hiyo itabidi hizo kata nyingine zisubiri hadi tutakapoambiwa mambo ni tayari,” alisema.

Akizungumza katika hafla hiyo fupi iliyofanyika Ikulu ndogo mjini Mpanda, Bw. Kiswaga alisema walikubali kutoa msaada huo kwa sababu wanamfahamu Waziri Mkuu Pinda kama mtu ambaye amekuwa akiendesha mashindano ya mpira mara kwa mara ili kudumisha umoja.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
DAR ES SALAAM
IJUMAA, MEI 15, 2009.

Read more...

WAZIRI MKUU PINDA AKATAZA POMBE KIJIJINI KWAO

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

WAZIRI MKUU PINDA AKATAZA POMBE KIJIJINI KWAO

*Azuia pia ngoma ya Chagulaga katika mojawapo ya kata za jimbo lake

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amepiga marufuku unywaji wa pombe katika siku za katikati ya wiki isipokuwa Jumapili tu ambayo ni siku ya mapumziko.

Ametoa onyo hilo alipokuwa katika siku ya pili ya ziara ya jimbo lake la Mpanda Mashariki wakati akiwahutubia wakazi wa Kata ya Kibaoni wilayani Mpanda ambako ni mahali alikozaliwa.

Akizungumza na wakazi hao, Waziri Mkuu aliwataka waache kunywa pombe kila siku na badala yake wajikite katika shughuli za kilimo ili waweze kuinua hali za maisha yao.

“Mkiitwa na Afisa Kilimo mnakwepa ... Tabia ya ngoja kwanza nikaonje lazima iishe. Pombe zote hakuna kuuzwa katikati ya wiki isipokuwa Jumapili na siku za sikukuu, ni lazima turudishe nidhamu ya kilimo bora, kilimo cha kufa na kupona,” alisema.

Alikemea tabia yao ya kukataa kutumia mvua za mwanzo za kupandia na kutoa visingizio mbalimbali na wakati wanapokuja kuzinduka msimu wa kupanda unakuwa umekwishapita.

Waziri Mkuu aliwapandisha jukwaani Afisa Kilimo wa Kata, Bw. Mathias Matogoro na Mtendaji wa Kijiji hicho, Bw. Ladislaus Nunguajua waeleze mbele ya mkutano huo wa hadhara walikuwa na ratiba gani kwa msimu unaoanza na walifanya nini katika msimu uliopita.

Akitoa maelezo yake, Afisa Kilimo Kata alisema alikuwa akiwahamasisha wakulima walime kilimo cha kisasa na kuwaelekeza katika shamba darasa la kijiji lakini waliohudhuria walikuwa wachache sana. Alisema amepanga kuwapeleka baadhi ya wakulima katika maonyesho ya nane nane ili wakirudi wawe chachu kwa wenzao.

Waziri Mkuu alimwambia Afisa huyo hana ya kuwapeleka kwenye maonyesho kwa sababu atapoteza muda na hao watakaorudi watakuwa wanasimulia maajabu ya mjini Sumbawanga. Badala yake alimtaka awasiliane na Halmashauri ya wilaya ya Mpanda ili awapeleke wakulima hao kwenye kituo kidogo cha mafunzo ya kilimo kilichopo Laela, wilayani Sumbawanga ambacho kinatoa mafunzo ya siku 14.

Naye Mtendaji wa Kijiji alipoulizwa ni kwa nini hakuwahimiza watu wake waende kwenye shamba darasa, alijibu kwamba wanakijiji waliofuatwa walikuwa wakitakaa na baada ya muda wanaenda kunywa pombe vilabuni.

Waziri Mkuu alisema hayo yote yanatokea kwa sababu ya viongozi kuchekeana na wananchi na ndiyo maana wanatoa visingizio na sababu ambazo haziishi. Aliwataka wawe makini katika kazi. “Ni lazima viongozi muanze kununa, hizi sababu na visingizia havitaisha …” alisema.

Mapema, akizungumza katika kijiji cha Kashishi kata ya Usevya, Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Kanali John Mzurikwao afuatilie kwa karibu usitishwaji wa ngoma hiyo kwa sababu inawadhalilisha wanawake.

“Nasikia bado mnaendelea kuicheza hii ngoma ya Chagulaga; nimewauliza akinamama hapa kama wanaipenda wengi wamesema hapana… ninamtuma DC alivalie njuga suala la ngoma ya chagulaga kwa sababu imepitwa na wakati, haifai! Akinababa tusaidiane kuipiga vita…,” alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa na umati wa watu.

Ngoma ya ‘Chagulaga’ huchezwa wakati wa usiku na wanaume hutumia nafasi hiyo kuwakamata wasichana au wanawake ambao wamekuwa wakiwatamani kwa muda mrefu na kufanya nao mapenzi kwa nguvu. Ubakaji ni njia mojawapo ambayo inachangia kwa kasi maambukizi ya virusi vya UKIMWI

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, MEI 15, 2009.

Read more...

MSAFARA WA WAZIRI MKUU WAKWAMA NJIANI MARA TATU

Wednesday, May 13, 2009

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MSAFARA WA WAZIRI MKUU WAKWAMA NJIANI MARA TATU
*Ni kutokana na mvua na utelezi
*Aombwa na wananchi kupita barabara mbovu, akubali

MSAFARA wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ulichelewa wa zaidi ya saa tatu kufika kwenye kijiji cha Muze katika bonde la Rukwa kwa sababu ya kukwama njiani mara tatu kutokana na utelezi.

Tukio lilitokea jana asubuhi (Jumanne, Mei 12, 2009) wakati akitoka Sumbawanga mjini kwenda kijijini hapo kukagua SACCOS ya Muze na kuzungumza na wananchi akiwa njiani kwenda Mamba, wilayani Mpanda kwa ziara ya siku mbili jimboni kwake.

Katika hali ya kawaida, safari ya kutelemka bonde la Rukwa ingechukua saa moja au pungufu ya hapo. Baadhi ya magari yaliyonasa katika utelezi huo ni gari la RPC, gari la walinzi na la Wasaidizi wa Waziri Mkuu.

Utelezi huo ulitokana na mvua zilizonyesha usiku wa kuamkia jana huku barabara aliyopita ya Ntendo hadi Muze ikiwa imemwagiwa kifusi ambacho kilikuwa kimeanza kusambazwa lakini hakijashindiliwa. Barabara hiyo ina urefu wa kilometa 37 lakini sehemu korofi ilikuwa na umbali wa kilometa 15.

Meneja wa TANROADS wa mkoa wa Rukwa, Eng. Joseph Nyamhanga alisema barabara hiyo ilikuwa inafanyiwa ukarabati wa awali ili iweze kufikia kiwango cha barabara zilizo chini ya Mradi wa Kuzikarabati Barabara ili zipitike muda wote (Performance Based Management and Maintenance of Roads – PMMR) ambao ni wa miaka mitano.

Alisema katika mpango huo, barabara ikishajengwa, inakuwa chini ya uangalizi wa mkandarasi mmoja kwa miaka mitano ambaye atapaswa kuifanyia matengenezo katika kipindi chote cha mradi. Mkandarasi anayejenga barabara hiyo ni KMM Entrepreneurs Ltd.)

Akizungumza baada ya kufika Mamba katika jimbo lake, Waziri Mkuu alisema Serikali inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuufungua ukanda wa bonde la Rukwa ambao una kilometa za mraba 1,200 sawa na hekta 120,000 au ekari 300,000 ambazo zinatumika kuzalisha mazao mbalimbali kubwa likiwa mpunga na mahindi.

Alisema changamoto hiyo inakuwa ngumu zaidi kwa sababu ya milima ya Lyamba lya Mfipa ambayo inatenganisha bonde hilo na ukanda wa juu uliko mji wa Sumbawanga ambako kuna barabara kuu jambo linalowafanya wakulima na wafanyabiashara wapate taabu kusafirisha mazao hadi upande wa pili.

“Wakati tukishuka mlima huu, tumekuta magunia ya mpunga yakiwa yamelundikwa njiani kwa sababu malori (fuso) yanayosomba mizigo inabidi yabebe magunia machache yashushe njiani halafu yarudi tena bondeni kusomba mengine, yakimaliza yarudi kuchukua kidogo kidogo ule mzigo wa njiani ili yamalizie kupandisha mlima,” alisema.

Barabara nyingine zinazounganisha bonde hilo na ukanda wa juu ni za Miangalua – Kipeta yenye kilometa 60 na ya Kalambazite – Ilemba yenye kilometa 30 lakini zote zinapandisha mlima huo mkubwa wenye urefu wa mita 1,800 kutoka usawa wa bahari wakati bonde la ziwa Rukwa liko mita 800 kutoka usawa wa bahari.

Juzi, Waziri Mkuu alilazimika kupita barabara ya Kalambazite – Ilemba baada ya kuombwa na wakazi wa Sakalilo kufanya hivyo kwa sababu walimlalamikia kuwa wanalipa nauli ya sh. 10,000 kutoka Sumbawanga lakini wakifika kwenye mlima huo wanatelemeshwa kwenye mabasi na kuambiwa washuke kwa miguu.

Alisema ili barabara hizo ziwe na manufaa, itabidi zipandishwe daraja na kuwa za mkoa ili ziweze kuhudumiwa kikamilifu kwani hivi sasa hizo ziko chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ambayo haiwezi kumudu gharama za matengenezo.

Alisema katika miinuko mikali ambayo haizidi kilometa moja, barabara za mlima huo zitahitaji kuwekewa lami au zege katika maeneo korofi ili zisiendelee kuharibika na hivyo kuondoa kikwazo cha usafiri kwa wananchi waishio bondeni.

Changamoto nyingine inayolikabili bonde la Rukwa linaloanzia kata za Kipeta, Mtowisa hadi Majimoto ni ukosefu wa daraja katika mto Momba ambao unaunganisha wilaya za Sumbawanga, Rukwa na Mbozi, mkoani Mbeya. Baadhi ya wananchi waliiomba Serikali ijenge daraja kubwa kuliko lililopangwa kujengwa sasa ili magari ya mizigo yaweze kupita na kukuza biashara katika bonde hilo.

Leo Waziri Mkuu atafanya mikutano ya hadhara katika kata za Majimoto, Mbede, Usevya, Kashishi na Kibaoni kabla ya kurejea Mpanda Mjini. Anatarajiwa kurejea jijini Dar es salaam kesho mchana.


(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, MEI 13, 2009.

Read more...

NAWAPA SIKU 90 KUKAMILISHA MICHANGO YA MAJI - PINDA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

NAWAPA SIKU 90 KUKAMILISHA MICHANGO YA MAJI - PINDA
*Asema wasipokamilisha, mradi uhamishiwe kijiji kingine

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewapa miezi mitatu wakazi wa kijiji cha Kilyamatundu kata ya Kipeta wawe wamekamilisha kutoa michango kwa ajili ya mradi wa maji safi la sivyo utahamishiwa katika kijiji kingine.

Alitoa kauli hiyo jana mchana (Jumatatu, Mei 11, 2009) wakati akihutubia mkutano wa hadhara na kujibu maswali ya wakazi wa kata hiyo ambako alikuwa katika siku ya pili ya kukagua shughuli za maendeleo wilayani Sumbawanga, mkoani Rukwa.

Waziri Mkuu alishangazwa na ugumu wa wakazi hao kuchelewa kukamilisha michango wakati wana mifugo mingi na wamevuna mpunga kwa wingi, jambo ambalo alisema lingeweza kuwasaidia kumudu michango ya sh. 2,000 kila mwanakijiji.

“Serikali imetenga sh. milioni 150 kwa ajili ya mradi huu. Haiwezekani tangu mwaka 2004 muwe mmechangia sh. 500,000 tu… sisi kama Serikali tunaandaa mipango na tunataka umiliki wa wananchi katika miradi kama hii, ndiyo maana mnaombwa mchangie asilimia tano tu ya gharama zote ambayo ni sh. milioni 7.5/-,” alisema.

Alisema kuna vijiji zaidi ya 100 katika wilaya hiyo ambavyo vinahitaji kupatiwa miradi ya maji safi lakini ni vijiji 10 tu ambavyo viliteuliwa kupatiwa mradi huo. “Huu ni mwezi Mei, ifikapo Agosti 31, kama hawajakamilisha michango yao, Mkurugenzi warudishie michango yao, na upeleke huu mradi kwenye kijiji kingine,” alisema Waziri Mkuu.

Akijibu maswali ya wananchi, Waziri Mkuu aliwaagiza Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Bw. Thobias Sijabaje na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Bw. Mussa Zungiza wafuatilie madai ya ujenzi hafifu wa shule ya sekondari ambayo wananchi walisema ujenzi wake umelipuliwa. “DC wenu ni mpya lakini itabidi aje na Mkurugenzi watafute ni kwa nini hadhi ya majengo hailingani na thamani halisi ya fedha,” alisema.

Akijibu maombi yao ya kupatiwa mradi wa umwagiliaji kwenye kutoka mto Momba unaomwaga maji yake katika ziwa Rukwa, Waziri Mkuu aliwaagiza viongozi wa halmashauri hiyo wafuatilie kama mradi huo upo na kama ulishafanyiwa upembuzi yakinifu kama wananchi hao wanavyodai.
Leo Waziri Mkuu anaanza ziara ya siku mbili katika jimbo lake la Mpanda Mashariki kwa kutembelea kata za Muze na Mamba ambako atafanya mikutano ya hadhara na kukabidhi kasiki ya kutunzia fedha kwa SACCOS ya Muze.


(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, MEI 12, 2009.

Read more...

ACHENI KULISHA MIFUGO KWENYE MABONDE YA KILIMO - PINDA

12 Mei, 2009

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

ACHENI KULISHA MIFUGO KWENYE MABONDE YA KILIMO - PINDA
*Aonya mifugo kupitishwa barabarani


WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewaonya wafugaji walioko kwenye bonde la ziwa Rukwa waache kuingiza mifugo yao kwenye mabonde ya umwagiliaji kwa vile inaharibu miundombinu katika miradi hiyo.

Alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Mei 11, 2009) wakati akiwahutubia wakazi wa kata ya Ilemba wilayani Sumbawanga, mkoani Rukwa mara baada ya kukagua skimu ya umwagiliaji ya Sakalilo.

“Katika hali ya kawaida, hili bonde lenye hekta 4,000 siyo la kulisha ng’ombe au mbuzi bali ni la kulima mazao ya chakula, mkiligeuza kuwa la malisho mtakuwa vichaa,” alisema huku akishangiliwa na wakazi hao.

Alisema mifugo ni lazima itengewe maeneo yake ya malisho na kukiri kuwa serikali ilifanya makosa kuruhusu mifugo iingie kwenye mabonde ya kilimo. “Tunatumia fedha nyingi sana kujenga miundombinu halafu unakuta mfugaji anaingiza mifugo ambayo siyo tu inakula mazao lakini pia inaharibu mifereji ambayo imegharimiwa na Serikali,” alisema.

Alisema wafugaji wengi wanachojali wao ni ng’ombe kushiba na siyo uharibifu unaotokana na matendo yao. Bonde la Rukwa ni miongoni mwa maeneo nchini yaliyoathiriwa na uhamiaji wa wafugaji kutoka mikoa ya Mwanza na Shinyanga.

Akizungumzia ufanisi wa skimu hiyo, Waziri Mkuu aliwataka wakazi hao wahakikishe kuwa wanazalisha magunia 30 ya mpunga kwa kila ekari na magunia 20 – 25 kwa kila ekari ya mahindi ili kweda sambamba na mpango wa kuleta mapinduzi ya kilimo mkoani Rukwa (MAKIRU).

“Hii ni skimu ni nzuri na mmeanza na ekari 500 si haba ni mwanzo mzuri, lakini kikubwa na wakulima kuwasumbua mabwanashamba... mfuate umuulize nataka kupata magunia 30 ya mpunga kwa ekari moja nifanyeje? Vivyo hivyo, kwa wanaolima mahindi, mwambie bwana shamba nataka kuvuna magunia 25 katika eka yangu, nitumie njia gani?” alifafanua.
Aliwaonya wafugaji wanaopitisha mifugo yao kwenye barabara kwani kwa kufanya hivyo ni kuharibu miundombinu hiyo na pia ni kinyume cha sheria ya nchi.

“Ni sheria ya nchi inayokataza mifugo kupitishwa kwenye barabara lakini pia ni gharama sana kuzikarabati barabara hizi kila mwaka... ninawasihi sana msirihusu mifugo kupita katikati ya barabara, watengenezeeni njia zao huko pembeni.”

Alisema ukarabati wa barabara ya kutoka Ilemba hadi Mamba unaofanyika hivi sasa una nia ya kufungua bonde la Rukwa ili uzalishaji unaofanyika ulete tija kwa wakulima wa bonde hilo.

Aliwasisitizia haja ya kuwa na ghala ili waweze kuanzisha mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani ambapo mkulima huweka mazao yake katika na kulipwa wakati wa mavuno na SACCOS huku akisubiri bei ipande ili mazo hayo yauzwe na kupatiwa malipo mara ya pili kutokana namavuno yaleyale.

Katika harambee ya papo kwa papo kuchangia ujenzi wa ghala hiyo, Waziri Mkuu alichangisha sh. milioni 14.47 kutoka kwa wajumbe aliofuatana nao kwenye msafara wake na kuahidi kufuatilia ili kuhakikisha wanafanikiwa. Alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha wanaanza kujenga ghala hilo katika muda usiozidi miezi sita.

Mapema akisoma taarifa ya skimu hiyo, Bwana shamba wa skimu hiyo Bw. Zurubabeli Matimba alimweleza Waziri Mkuu kwamba skimu hiyo inakabiliwa na mmomonyoko wa udongo kutokana na mifugo inayoingizwa kwenye skimu hiyo kinyume cha taratibu.

Alisema changamoto nyingine inayowakabili ni uelewa mdogo miongoni mwa wakulima juu ya kilimo bora cha mpunga kwani wengi hutumia zaidi mbegu za asili ambazo hazikawii kuanguka upepo unapozidi.

Leo Waziri Mkuu anaanza ziara ya siku mbili katika jimbo lake la Mpanda Mashariki kwa kutembelea kata za Muze na Mamba ambako atafanya mikutano ya hadhara na kukabidhi kasiki ya kuhifadhia fedha kwa SACCOS ya Muze.


(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, MEI 12, 2009.

Read more...

PINDA: UONGOZI BORA INABIDI UANGALIWE UPYA

Sunday, May 10, 2009

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

PINDA: UONGOZI BORA INABIDI UANGALIWE UPYA

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema kati ya mambo manne ambayo hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere aliwafundisha Watanzania, uongozi bora ni jambo linalohitaji kutazamwa kwa umakini zaidi.

Akizungumza na Wakuu wa Mikoa sita ya Morogoro, Iringa, Mbeya, Ruvuma, Kigoma na Rukwa na Wakuu wa Wilaya zao kwenye mkutano wa majumuisho ya ziara zake katika mikoa hiyo uliofanyika jana (Jumamosi, Mei 9, 2009) mjini Sumbawanga, Rukwa, Waziri Mkuu alisema kutokana na mjadala wa kikao hicho hana hakika kama uongozi bora bado upo.

“Mwalimu Nyerere alisema ili tuendelee tunahitaji mambo manne muhimu ambayo ni Ardhi, Watu, Siasa Safi na Uongozi Bora. Katika mikoa hii sita mambo matatu ya mwanzo nina uhakika yapo, je uongozi bora tunao? Sina hakika lakini mjadala umeonyesha ni lazima turekebishe hali iliyopo,” alisema.

Alisema ardhi ipo na watu wapo na hata siasa safi kuhusu Kilimo imewekwa bayana na kwa kina katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2005, Sura ya Tatu kuanzia ukurasa wa 22 hadi wa 46 ambapo kwa sentensi moja Ilani inasema “Kilimo cha Kisasa ndio Msingi wa Uchumi wa Kisasa.”

Alisema Ilani ya CCM imebainisha matatizo ya kilimo cha Tanzania ambayo mengi amekutana nayo katika ziara hiyo. Alitaja baadhi ya matatizo hayo kuwa ni: Wakulima wengi kutojua na kutotekeleza kanuni za kilimo bora za mazao wanayoyalima hivyo kilimo chao kukosa tija na mavuno yao kuwa kidogo; Wakulima wengi kulima vishamba vidogo vidogo na kutegemea zana duni za jadi na hasa jembe la mkono.

Aliyataja matatizo mengine kuwa ni upatikanaji wa mbegu bora na mbolea kutokuwa na mfumo wa uhakika na matumizi yake kutoenezwa kwa wakulima; kazi nyingi za kilimo kutegemea nguvukazi ya binadamu hasa ya wanawake na kuacha maji ya mvua yaendelee kwenda baharini au kwenye maziwa badala ya kuyakinga kwenye visima, malambo na mabwawa kwa matumizi ya watu, mifugo na kilimo cha umwagiliaji.

Waziri Mkuu alisema matatizo yote haya yanahitaji kiongozi bora ili yapatiwe ufumbuzi. “Hapa tunahitaji viongozi wanaojituma kuwasaidia wananchi waondokane na umaskini. Wawe ni watu wanaochukia hali ya umaskini walionao wananchi wengi; wanaojinyima kutumia Bajeti ya Serikali kwa kujinufaisha bali kwa kununua zana za kilimo na kuongeza huduma kwa wakulima,” alisema huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano huo.

“Wanapaswa waongoze kwa mfano, kwa maana ya kuwa na mashamba yanayohudumiwa kitaalam na yenye kuwa na uzalishaji wenye tija... Ili kuleta mapinduzi ya kilimo, ni vizuri viongozi wawe na mashamba yao ya mfano ili wananchi waige kutoka kwao. Hizi ni sifa muhimu anazotakiwa kuwa nazo kiongozi katika ngazi zote ili kuweza kutekeleza kikamilifu Maazimio ya Mkutano wa Morogoro,” alisisitiza Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu aliitisha kikao hicho cha majumuisho akitaka Wakuu wa Wilaya wamweleze wametekeleza vipi maazimio 21 yaliyofikiwa katika mkutano aliouitisha mjini Morogoro Oktoba 16 -18, 2008 kuweka malengo ya kuinua kilimo katika mikoa sita ya Morogoro, Iringa, Mbeya, Ruvuma, Kigoma na Rukwa. Pia alitaka Wakuu wa Mikoa hiyo sita waelezee changamoto za jumla katika mikoa yao kwenye sekta ya kilimo na jinsi walivyojipanga kukabiliana nazo.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Waziri wa Nchi (OWM-TAMISEMI), Bi. Celina Kombani; Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Dk. Mathayo David; Naibu Waziri wa Fedha, Bw. Jeremiah Sumari; na Wakurugenzi kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji; Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.

Makundi mengine yaliyohudhuria mkutano huo ni wabunge wanne wa mkoa wa Rukwa, baadhi ya makatibu tawala wa mikoa, baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri, washauri wa kilimo wa kila mkoa na makatibu wa CCM kutoka kila mkoa.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, MEI 10, 2009.

Read more...

Waziri Mkuu


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na mkewe Tunu wakipata maelezo kutoka kwa Rose Mongi (kulia) ambaye ni mtaalamu wa utafiti wa mbegu bora katika kituo kidogo cha utafiti cha Milundikwa wilayani Nkasi, mkoani Rukwa kuhusu utafiti wa mbegu bora za ngano wakati walipotembelea shamba la kituo hicho juzi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Read more...

About This Blog

Blog Archive

  © Blogger template Noblarum by Ourblogtemplates.com 2009

Back to TOP