WAZIRI MKUU PINDA AKATAZA POMBE KIJIJINI KWAO
Friday, May 15, 2009
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI MKUU PINDA AKATAZA POMBE KIJIJINI KWAO
*Azuia pia ngoma ya Chagulaga katika mojawapo ya kata za jimbo lake
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amepiga marufuku unywaji wa pombe katika siku za katikati ya wiki isipokuwa Jumapili tu ambayo ni siku ya mapumziko.
Ametoa onyo hilo alipokuwa katika siku ya pili ya ziara ya jimbo lake la Mpanda Mashariki wakati akiwahutubia wakazi wa Kata ya Kibaoni wilayani Mpanda ambako ni mahali alikozaliwa.
Akizungumza na wakazi hao, Waziri Mkuu aliwataka waache kunywa pombe kila siku na badala yake wajikite katika shughuli za kilimo ili waweze kuinua hali za maisha yao.
“Mkiitwa na Afisa Kilimo mnakwepa ... Tabia ya ngoja kwanza nikaonje lazima iishe. Pombe zote hakuna kuuzwa katikati ya wiki isipokuwa Jumapili na siku za sikukuu, ni lazima turudishe nidhamu ya kilimo bora, kilimo cha kufa na kupona,†alisema.
Alikemea tabia yao ya kukataa kutumia mvua za mwanzo za kupandia na kutoa visingizio mbalimbali na wakati wanapokuja kuzinduka msimu wa kupanda unakuwa umekwishapita.
Waziri Mkuu aliwapandisha jukwaani Afisa Kilimo wa Kata, Bw. Mathias Matogoro na Mtendaji wa Kijiji hicho, Bw. Ladislaus Nunguajua waeleze mbele ya mkutano huo wa hadhara walikuwa na ratiba gani kwa msimu unaoanza na walifanya nini katika msimu uliopita.
Akitoa maelezo yake, Afisa Kilimo Kata alisema alikuwa akiwahamasisha wakulima walime kilimo cha kisasa na kuwaelekeza katika shamba darasa la kijiji lakini waliohudhuria walikuwa wachache sana. Alisema amepanga kuwapeleka baadhi ya wakulima katika maonyesho ya nane nane ili wakirudi wawe chachu kwa wenzao.
Waziri Mkuu alimwambia Afisa huyo hana ya kuwapeleka kwenye maonyesho kwa sababu atapoteza muda na hao watakaorudi watakuwa wanasimulia maajabu ya mjini Sumbawanga. Badala yake alimtaka awasiliane na Halmashauri ya wilaya ya Mpanda ili awapeleke wakulima hao kwenye kituo kidogo cha mafunzo ya kilimo kilichopo Laela, wilayani Sumbawanga ambacho kinatoa mafunzo ya siku 14.
Naye Mtendaji wa Kijiji alipoulizwa ni kwa nini hakuwahimiza watu wake waende kwenye shamba darasa, alijibu kwamba wanakijiji waliofuatwa walikuwa wakitakaa na baada ya muda wanaenda kunywa pombe vilabuni.
Waziri Mkuu alisema hayo yote yanatokea kwa sababu ya viongozi kuchekeana na wananchi na ndiyo maana wanatoa visingizio na sababu ambazo haziishi. Aliwataka wawe makini katika kazi. “Ni lazima viongozi muanze kununa, hizi sababu na visingizia havitaisha …†alisema.
Mapema, akizungumza katika kijiji cha Kashishi kata ya Usevya, Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Kanali John Mzurikwao afuatilie kwa karibu usitishwaji wa ngoma hiyo kwa sababu inawadhalilisha wanawake.
“Nasikia bado mnaendelea kuicheza hii ngoma ya Chagulaga; nimewauliza akinamama hapa kama wanaipenda wengi wamesema hapana… ninamtuma DC alivalie njuga suala la ngoma ya chagulaga kwa sababu imepitwa na wakati, haifai! Akinababa tusaidiane kuipiga vita…,†alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa na umati wa watu.
Ngoma ya ‘Chagulaga’ huchezwa wakati wa usiku na wanaume hutumia nafasi hiyo kuwakamata wasichana au wanawake ambao wamekuwa wakiwatamani kwa muda mrefu na kufanya nao mapenzi kwa nguvu. Ubakaji ni njia mojawapo ambayo inachangia kwa kasi maambukizi ya virusi vya UKIMWI
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, MEI 15, 2009.
0 comments:
Post a Comment