PINDA: UONGOZI BORA INABIDI UANGALIWE UPYA
Sunday, May 10, 2009
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
PINDA: UONGOZI BORA INABIDI UANGALIWE UPYA
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema kati ya mambo manne ambayo hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere aliwafundisha Watanzania, uongozi bora ni jambo linalohitaji kutazamwa kwa umakini zaidi.
Akizungumza na Wakuu wa Mikoa sita ya Morogoro, Iringa, Mbeya, Ruvuma, Kigoma na Rukwa na Wakuu wa Wilaya zao kwenye mkutano wa majumuisho ya ziara zake katika mikoa hiyo uliofanyika jana (Jumamosi, Mei 9, 2009) mjini Sumbawanga, Rukwa, Waziri Mkuu alisema kutokana na mjadala wa kikao hicho hana hakika kama uongozi bora bado upo.
“Mwalimu Nyerere alisema ili tuendelee tunahitaji mambo manne muhimu ambayo ni Ardhi, Watu, Siasa Safi na Uongozi Bora. Katika mikoa hii sita mambo matatu ya mwanzo nina uhakika yapo, je uongozi bora tunao? Sina hakika lakini mjadala umeonyesha ni lazima turekebishe hali iliyopo,†alisema.
Alisema ardhi ipo na watu wapo na hata siasa safi kuhusu Kilimo imewekwa bayana na kwa kina katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2005, Sura ya Tatu kuanzia ukurasa wa 22 hadi wa 46 ambapo kwa sentensi moja Ilani inasema “Kilimo cha Kisasa ndio Msingi wa Uchumi wa Kisasa.â€
Alisema Ilani ya CCM imebainisha matatizo ya kilimo cha Tanzania ambayo mengi amekutana nayo katika ziara hiyo. Alitaja baadhi ya matatizo hayo kuwa ni: Wakulima wengi kutojua na kutotekeleza kanuni za kilimo bora za mazao wanayoyalima hivyo kilimo chao kukosa tija na mavuno yao kuwa kidogo; Wakulima wengi kulima vishamba vidogo vidogo na kutegemea zana duni za jadi na hasa jembe la mkono.
Aliyataja matatizo mengine kuwa ni upatikanaji wa mbegu bora na mbolea kutokuwa na mfumo wa uhakika na matumizi yake kutoenezwa kwa wakulima; kazi nyingi za kilimo kutegemea nguvukazi ya binadamu hasa ya wanawake na kuacha maji ya mvua yaendelee kwenda baharini au kwenye maziwa badala ya kuyakinga kwenye visima, malambo na mabwawa kwa matumizi ya watu, mifugo na kilimo cha umwagiliaji.
Waziri Mkuu alisema matatizo yote haya yanahitaji kiongozi bora ili yapatiwe ufumbuzi. “Hapa tunahitaji viongozi wanaojituma kuwasaidia wananchi waondokane na umaskini. Wawe ni watu wanaochukia hali ya umaskini walionao wananchi wengi; wanaojinyima kutumia Bajeti ya Serikali kwa kujinufaisha bali kwa kununua zana za kilimo na kuongeza huduma kwa wakulima,†alisema huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano huo.
“Wanapaswa waongoze kwa mfano, kwa maana ya kuwa na mashamba yanayohudumiwa kitaalam na yenye kuwa na uzalishaji wenye tija... Ili kuleta mapinduzi ya kilimo, ni vizuri viongozi wawe na mashamba yao ya mfano ili wananchi waige kutoka kwao. Hizi ni sifa muhimu anazotakiwa kuwa nazo kiongozi katika ngazi zote ili kuweza kutekeleza kikamilifu Maazimio ya Mkutano wa Morogoro,†alisisitiza Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu aliitisha kikao hicho cha majumuisho akitaka Wakuu wa Wilaya wamweleze wametekeleza vipi maazimio 21 yaliyofikiwa katika mkutano aliouitisha mjini Morogoro Oktoba 16 -18, 2008 kuweka malengo ya kuinua kilimo katika mikoa sita ya Morogoro, Iringa, Mbeya, Ruvuma, Kigoma na Rukwa. Pia alitaka Wakuu wa Mikoa hiyo sita waelezee changamoto za jumla katika mikoa yao kwenye sekta ya kilimo na jinsi walivyojipanga kukabiliana nazo.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Waziri wa Nchi (OWM-TAMISEMI), Bi. Celina Kombani; Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Dk. Mathayo David; Naibu Waziri wa Fedha, Bw. Jeremiah Sumari; na Wakurugenzi kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji; Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
Makundi mengine yaliyohudhuria mkutano huo ni wabunge wanne wa mkoa wa Rukwa, baadhi ya makatibu tawala wa mikoa, baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri, washauri wa kilimo wa kila mkoa na makatibu wa CCM kutoka kila mkoa.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, MEI 10, 2009.
0 comments:
Post a Comment