WAZIRI MKUU ASEMA KILIMO KINATAKA NIDHAMU

Sunday, May 10, 2009

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

WAZIRI MKUU ASEMA KILIMO KINATAKA NIDHAMU
*Ataka Ma-RC na DC wapige marufuku watu kulima hovyo
*

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema kazi ya kilimo inataka nidhamu ya hali ya juu ili maisha ya Mtanzania yawe ni zaidi ya kula na kushiba na kuweza kumudu mahitaji mengine ya kiuchumi.

Alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Wakuu wa Mikoa sita na Wakuu wa Wilaya zao kwenye mkutano wa majumuisho ya ziara zake katika mikoa hiyo uliofanyika jana (Jumamosi, Mei 9, 2009) mjini Sumbawanga, Rukwa.

Alisema wataalamu wakikaa kwa haraka na kuona kwamba watu wanakula na kulala watasema kuwa watu wana maisha bora lakini wanaotaka kujua ukweli wa mambo waende kumtazama mtu wa kijijini.

“Sie hapa tunaweza kubishana kuhusu kauli za wakubwa kwamba Watanzania wanaishi chini ya dola moja kwa siku lakini ukitaka kuujua ukweli uende kumtazama mtu wa kijijini... huyu ukimwangalia utasema mbona anakula ugali na maharage kila siku, ana nyumba ya kuishi, lakini kikubwa hapa ni kipato cha mfukoni.”

“Hii haitoshi, huyu mtu anapaswa awe na pesa ya kupeleka watoto shule, kununulia sabuni au sukari haya hayawezi kupatikana kama mtu anaishi kwa sh. 1,200 kwa siku.”

“Hapa napenda nisisitize, maisha ya Mtanzania yanapaswa yawe ni zaidi ya kula, aweze kumudu na vitu vingine katika maisha,... sisi kama viongozi tukiweza kubadili maisha ya huyu mtu akaweza kufika hapo ndiyo tutakuwa tumemsaidia huyu Mtanzania kuishi maisha bora.”

Alisema nchi kama China na Vietnam zimeweza kufika mbali kwa sababu ya kuweka nidhamu katika kilimo. Aliwataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wapige marufuku watu kulima bila kufuta kanuni bora za kilimo. “Pigeni marufuku watu kulima hovyo, tuanze sasa kujipanga vizuri kwa msimu unaofuata, ” alisisitiza.

Akichambua kipato cha Mtanzania kwa kuangalia Pato la Mwananchi (GDP per capita) kwa mwaka 2007, Waziri Mkuu aliwatajia vipato vya wakazi wa mikoa hiyo sita na nafasi zao kitaifa na kusema mkoa wa Iringa ndiyo unaongoza katika kundi hilo kwa kuwa na wastani wa sh. 617,448 huku ikishika nafasi ya pili kitaifa.

Alisema mkoa mkoa wa pili katika kundi hilo ni Ruvuma ambao wastani wake ni sh. 599,794 kwa mwaka 2007 huku ikishika nafasi ya tatu kifaifa wakati mkoa wa tatu ni Mbeya yenye wastani wa pato la sh. 560,773 huku ikishika nafasi ya saba kitaifa. Mkoa wa Morogoro ni wa nne katika kundi hilo kwa wastani wa sh. 520,018 huku ikishika nafasi ya tisa kitaifa na Rukwa ni wa tano kwa kuwa na wastani wa sh. 486,832 huku ikiwa na 11 kitaifa wakati Kigoma ni wa mwisho kwa kuwa na wastani wa sh. 360,290 huku ikiwa ni ya 19 kitaifa.
ANGALIZO:
S/NO
MKOA
GDP
NAFASI KITAIFA
1.
IRINGA
Sh. 617,448
2
2.
RUVUMA
Sh. 599,794
3
3.
MBEYA
Sh. 560,773
7
4.
MOROGORO
Sh. 520,018
9
5.
RUKWA
Sh. 486,832
11
6.
KIGOMA
Sh. 360,290
19


Akibainisha zaidi, Waziri Mkuu alisema wastani wa pato la mwananchi kitaifa kwa mwaka 2007 lilikuwa ni sh. 495,932 huku mkoa wa Dar es Salaam ukiongoza kwa kuwa na pato la mwananchi linalofikia wastani wa sh. 1,027,526 zaidi ya mara mbili ya wastani wa kitaifa na Mkoa wa Singida ukiwa wa mwisho kwa kuwa na kipato cha sh. 277,078, chini ya nusu ya wastani wa kitaifa.

“Alisema mikoa iliyoongoza katika kundi hilo ya Iringa, Ruvuma, Mbeya, inachangiwa na fursa walizonazo za miundombinu bora ambayo inasaidia hata usafirishaji wa mazao ya wakuliwa uwe mzuri na wa haraka. Wana mazao ya biashara kama chai, miwati, mpunga, tofauti na Kigoma au Rukwa ambao barabara limekuwa ni tatizo la muda mrefu.”

Alisema hata mkoa wa Morogoro haukupaswa kuwa wa nne katika kundi hilo au wa tisa kitaifa kwa saabu wenyewe una fursa nyingi ikilinganishwa na mikoa mingine na kutaja baadhi kuwa ni barabara, reli, ardhi nzuri ya kilimo, mito kwa ajili ya umwagiliaji, na ukaribu na jiji la Dar es Salaam ambako ndiko soko kubwa liliko.

Akizungumzia kiwango cha juu cha mkoa wa Dar es Salaam, Waziri Mkuu alisema wenyewe unaongoza kwa sababu una viwanda, miundombinu ya uhakika, umeme na uwekezaji uko juu na kuongeza kuwa hali hiyo si halisi kwa wananchi wa kawaida waishio Tandika au Manzese jijiji humo.

“Pamoja na tofauti kubwa ya Pato la Mwananchi katika mikoa hii sita hasa baina ya Iringa na Kigoma, bado fursa za kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo ni kubwa kwa sababu ni wazuri katika kilimo na ni wachapakazi. Lakini lazima tujiulize je wanachozalisha, kinawasaidiaje kuinua hali zao za maisha?”

Alisema kikubwa wanachohitaji ni kuwezeshwa ili waweze kuinuka na kutoka hapo walipo kwa hiyo kama kundi moja wanapaswa kushirikiana ili kutumia fursa zilizopo. “Kama wakulima watazingatia kanuni za kilimo bora, watazalisha kwa wingi na ziada ikiuzwa itaongeza pato la mwananchi kwa kiwango kikubwa,” aliongeza Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu aliitisha kikao hicho cha majumuisho akitaka Wakuu wa Wilaya wamweleze wametekeleza vipi maazimio 21 yaliyofikiwa katika mkutano aliouitisha mjini Morogoro Oktoba 16 -18, 2008 kuweka malengo ya kuinua kilimo katika mikoa sita ya Morogoro, Iringa, Mbeya, Ruvuma, Kigoma na Rukwa. Pia alitaka Wakuu wa Mikoa hiyo sita waelezee changamoto za jumla katika mikoa yao kwenye sekta ya kilimo na jinsi walivyojipanga kukabiliana nazo.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, MEI 10, 2009.

0 comments:

Post a Comment

About This Blog

Blog Archive

  © Blogger template Noblarum by Ourblogtemplates.com 2009

Back to TOP